Thursday, 12 January 2017

MKUU WA MKOA WA LINDI AWAASA WATUMISHI KUZINGATIA KANUNI NA SHERIA ZA UTUMISHI WA UMMA

Na: Mwanakheri Ally
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amewataka Watumishi wa Wilaya ya Ruangwa kuzingatia maadili na miiko ya Utumishi wa Umma

Mkuu wa Mkoa aliwausia Watumishi kwa kuwakumbusha wajibu wao na kuwaonya matumizi mabaya ya simu za mkononi wakati wa muda wa kazi, pia aliwaasa kuacha mazoea ya karibu na Wanafunzi ambayo yatapelekea mahusiano yasiyokuwa rasmi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Walimu wa Shule ya Sekondari Ruangwa wakati wa ziara yake ya kikazi aliyoifanya katika Wilaya hiyo tarehe 11/01/ 2017.

Pia aliwaambia Watumishi hasa wa kada ya Elimu kuwa wao ni Wazazi na Viongozi wa Jamii  inayowazunguka hivyo wanapaswa kuwa mfano mzuri wa kuingwa katika Jamii, na wanapaswa kuzingatia mavazi yenye maadili wanapokuwa maeneo ya kazi.

 Aidha, Mkuuhuyo wa Mkoa alimtaka Mkuu wa Wilaya  ya Ruangwa, Mhe. Joseph Mkirikiti kufuatilia Watoto wenye utoro sugu mashuleni kwa kuanza kuwakamata Wazazi wao na pia Watoto hao kuchukuliwa hatua kwa pamoja ili kuweza kufanikisha kutokomeza utoro mashuleni.

Vilevile aliutaka uongozi wa Halmshauri kuzingatia kujenga vyoo ambavyo havitumi maji mengi katika ujenzi wa shule mpya inayojengwa Wilayani hapo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, alisema ameanzisha mkakati wa kukabiliana na Watoto wenye utoro sugu kwa kuweka utaratibu wa kupelekewa idadi ya Wanafunzi watoro kila siku ya Jumatatu na utaratibu huuuinaanza mara moja.