WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya ziara katika hospitali ya wilaya ya Ruangwa na amekabidhi magari mawili ya kubebea wagonjwa.
Amesema kati ya
magari hayo moja ni kwa ajili ya hospitali hiyo ya wilaya na la pili
litapelekwa katika kituo cha afya cha Mandawa.
Waziri Mkuu amekabidhi magari hayo leo (Jumatano, Julai 12,
2017), alipotembelea hospitali hiyo, ikiwa ni siku ya tatu ya ziara yake ya kikazi Mkoani Lindi.
Amesema magari hayo ni
muendelezo wa mkakati wa Serikali ya awamu ya tano wa kuboresha huduma za afya
kwa wananchi wake.
“Rais wetu Dkt. John
Magufuli amedhamiria kuwaondolea wananchi kero mbalimbali zinazowakabili
zikiwemo za huduma za afya, hivyo tuendelee kumuunga mkono.”
Waziri Mkuu amesema magari
hayo ya kisasa yatasaidia kurahisisha usafiri kwa wagonjwa wanaohitaji
matibabu ya dharura katika hospitali kubwa.
Kabla ya
kukabidhi magari hayo, Waziri Mkuu alitembelea wodi ya akina mama
na ya watoto waliolazwa katika hospitali hiyo na amesema kwamba
ameridhishwa na hali ya utoaji huduma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Mheshimiwa
Rashid Nakumbya amesema magari hayo ni faraja kwao kwa kuwa walikuwa na
changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wa dharura.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi wakati alipo tembelea hospitali ya Wilaya Ruangwa, akiwa kwenye ziara ya kikazi |
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe wakati alipo kabidhi gari mbili za kisasa za kubebea wagonjwa,katika hospitali ya Wilaya Ruangwa, akiwa kwenye ziara ya kikazi ya siku nne Mkoani Lindi, |
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikagua gari ya kubebea wagonjwa wakati alipokabidhi gari mbili za kisasa za kubebea wagonjwa,katika hospitali ya Wilaya Ruangwa, akiwa kwenye ziara ya kikazi |
Gari la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa na Waziri Mkuu katika Hospitali ya Wilaya ya Ruangwa wakati wa Ziara yake ya kikazi |
Waziri Mkuu akisalimiana na Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya dr Bogia |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya akitoa neno la shukurani kwa Waziri Mkuu baada ya kukabidhiwa gari za kubebea wagonjwa mbili. |