Wednesday, 19 July 2017

Zambi: Atoa Pongezi Kwa Halmashauri Ya Ruangwa Kwa Kupata Hati Safi



Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kupata hati inayoridhisha  na kuweza kufuta hoja 123 mpaka kufikia hoja 15.

Hati inayoridhisha inatolewa wakati mkaguzi ameridhia kuwa hakuna dosari zozote katika hesabu, na taarifa za fedha zimeandaliwa kwa mujibu wa mfumo na viwango vya uandaaji taarifa za fedha zinavyokubalika Kitaifa na Kimataifa.

Mkuu wa Mkoa ametoa pongezi hizo wakati wa Mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani wa Kupitia hoja za Ukaguzi mwaka 2015/ 2016 katika ukumbi wa RUTESCO mjini Ruangwa.

Mhe Zambi alitoa pongezi kwa jitihada za menejmenti  ya Wilaya kwa kufanikiwa kufunga hojanyingi zilizokuwa zinaikabili Halmashauri hiyo.

“Halmashauri hii ndiyo ilikuwa inaongoza kwa hoja nyingi kuliko halmashauri zote za Mkoa wa Lindi sikutegemea kama zingeweza kupungua kwa kiasi hiki Menejmenti mmefanya kazi ya ziada hongereni sana” alisema Zambi.

Aidha aliwataka waheshimiwa Madiwani kuwasimamia wataalamu wa Halmashauri bila kuangalia ukaribu wao,mtu akikosea awajibishwe kama sheria na taratibu inavyotaka.

“Sheria na taratibu zinawekwa ili zifuate si hiari kwa Menejimenti na Madiwani kuzifuata. Maagizo ya serikali yakija ni wajibu wa madiwani na menejimenti kuyatekeleza kama yanavyoagiza”.

Naye Katibu Tawala Mkoa Ndugu Ramadhani Kaswa aliusisitiza uongozi wa Halmashauri kufanya manunuzi kwa wazabuni wenye risti za kielektroniki ili kuepuka hoja za namna hiyo.

Pia alisema zipo njia nyingi za kuepuka hoja mbalimbali zinazokuwa zinajirudia kila mwaka, Halmashauri inatakiwa ipunguze kukopa huduma ili kuepuka hoja,  inatakiwa matumizi yafanyike kutokana na bajeti iliyokuwepo.

Naye M wenyekiti wa Halmashauri Rashidi Nakumbya aliwataka waheshimiwa madiwani kusimama katika kata zao ilikuweza kumaliza viporo vya majengo vilivyokuwepo kwa kuwashirikisha wananchi wao.

“tukiwashirikisha wananchi kwenye kata zetu haya majengo viporo tutayamaliza, Halmashauri ina majukumu mengi tukitegemea itumalizie matatizo yote katika kata zetu tutachelewa tujitoea na wananchi wetu kufanikisha ahadi tulizoziweka za kuwatumikia wananchi”alisema  Nakumbiya


Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Andrea Chezue akimkaribisha Mwenyekiti wa Halmashauri aendelee na taratibu nyingine

Mwenyekiti wa Halmashauri akifungua kikoa maalum cha baraza kilichofanyika 15/07/2017

Wataalamu wakiwa wanafuatilia mjadala kwa umakini wa kikao

Madiwani wakiwa wanamsikiliza Mkaguzi wa  Fedha za Serikali akiwasilisha taarifa yake kwa Mkuu wa Mkoa

Mkanguzi wa Fedha za Serikali Nyaulingo akiwasilisha Taaarifa kwenye kikao cha Baraza

(kushoto) Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi na (Katikati) ni Katibu Tawala Mkoa Ramadhani Kaswa na kulia) Makamu mwenyekiti wa Halmashauri

Mhe wa Diwani wa Kata ya Ruangwa Pendeka Kakiuliza swali baada ya taarifa kuwasilishwa katika kikao hiko

Katibu Tawala Mkoa akizungumza na menejmenti na waheshimiwa Madiwani na kuelekeza njia za kumaliza hoja zilizobaki

Mkuu wa Wilaya Joseph Mkirikiti akizungumza katika kikoa maalumu cha Baraza la Madiwani


Wakuu wa idara wakiwa wanamsikiliza kwa umakini maagizo ya Mkuu wa Mkoa

Wageni kutoka mkoani waliohudhuria kikao hiko maalumu cha Baraza la Madiwani

Mkuu wa Mkoa wa Lindi Godfrey Zambi akihutubia Baraza la Madiwani


Mkuu wa Mkoa akitoa msisitizo wa kufuata maagizo yanayotoka serikali kuu